Jumatatu , 19th Oct , 2020

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Ilala  imefanikiwa kumkamata Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi laki moja (100,000) kinyume sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Akizungumzia Mapema leo, jijini Dar es salaam, na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya utendaji wa Takukuru mkoa wa Ilala kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, 2020, Kamanda wa Takukuru, Ilala, Christopher Myava, amesema  mwenyekiti huyo alifanya kosa hilo ili kamati ya serikali ya mtaa iweze kumjadili na kumpitisha mtoa taarifa kwenye maombi ya kumiliki silaha ambapo uchunguzi wa shauri hilo uko katika hatua za mwisho ili liweze kufikishwa mahakamani.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mayava, amesema wameweza kudhibiti upotevu wa fedha kiasi Cha Tsh. 35,643,000 kutoka kwa wadaiwa Sugu wa vikoba ,Saccos na fedha  husika kupatiwa Sacco's na vikoba husika.

Akizungumzia juu ya kuelekea uchaguzi mkuu  amesema bado hawajapata kesi yoyote ya vitendo vya rushwa kwa mkoa huo huku akidai kuwa wanaendelea kufuatilia na kutoa elimu.