Kiungo mshambuliaji wa timu ya Simba akipambana na wachezaji wa timu ya Mtibwa Sukar.
Mdudu wa matokeo ya Sare ameendelea kuwaandama wekundu wa msimbazi Simba SC baada ya hii leo kujikuta wakitoka sare ya Sita mfululizo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar, katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro jioni ya leo.
Ushindi huo, unawafanya Mtibwa wafikishe pointi 14 kileleni mwa ligi hiyo, wakati Simba SC imefikisha pointi 6.
Matokeo hayo ni kama kufeli kwa mtihani wa kwanza kwa benchi la ufundi la Simba chini ya kocha Patrick Phiri ambao walipewa michezo miwili ya kuhakikisha timu hiyo inaibuka na ushindi huku ikicheza soka safi na la kuvutia.
Simba SC ilikwenda kupumzika ikiwa tayari inaongoza kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na beki wa kimataifa wa Uganda, Joseph Owino dakika ya 35 kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Emmanuel Okwi, Na dakika chache kabla ya kwenda mapumziko beki wa kushoto wa mtibwa David Luhende akikosa mkwaju wa penati baada ya shuti lake kupanguliwa na mlinda mlango kinda wa Simba Manyika Peter
Na katika kipindi cha pili vinara wa hao wa Ligi Kuu wapate bao la kusawazisha dakika ya 58, mfungaji Mussa Hassan Mgosi aliyetumia makosa ya beki wa kulia, William Lucian ‘Gallas’ kuchanganyana na kipa wake, Manyika Jr.
Mtibwa Sugar: Said Mohammed, Hassan Ramadhani, David Luhende, Andrew Vincent, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Mussa Ngosi, Mohamed Ibrahim, Ame Ally, Mussa Nampaka na Ally Shomary
Simba SC: Peter Manyika, William Lucian ‘Gallas’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Awadh Juma, Elias Maguri/Amisi Tambwe dk76, Said Ndemla na Emmanuel Okwi/Uhuru Suleiman dk75.
Nao Yanga wameshinwa kuendeleza wimbi la ushindi katika michezo yao ya kanda ya ziwa mara baada ya hii leo kukubali kichapo cha bao 1-0 toka kwa wanankurukumbi timu ya wakata miwa wa Kagera Sugar kwa bao pekee la kiungo Paul Ngway kunako dakika ya 52 mchezo ukipigwa katika dimba la Kaitaba, Bukoba.
Na katika mchezo huo Yanga SC ilimaliza mchezo huo pungufu, baada ya Nahodha wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 80 na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, baada ya kumpiga kiwiko mchezaji Rashid Mandawa wa Kagera Sugar
Baada ya mchezo huo, mashabiki wa Yanga SC walimtisha refa kiasi cha kutolewa uwanjani kwa msaada wa askari wa Polisi.
Kagera Sugar: Agathon Anthony, Benjamin Asukile, Abubakar Mtiro, Erick Kyaruzi, George Kavilla, Babu Ally, Julius Ambrose, Paul Maona, Rashid Mandawa, Atupele Green na Adam Kingwande
Yanga SC: Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Genilson Santos ‘Jaja’, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho
Wakati hayo yakiendelea kwa vigogo vya soka hapa nchini Simba na Yanga nao mabingwa wa tetezi wa ligi kuu Tanzania bara Azam fc wamejikuta wakipokea kichapo cha pili mfululizo mara baada ya hii leo ikiwa ugenini kukubali kichapo cha bao 1-0 toka kwa timu ya Ndanda FC ya Mtwara katika mchezo uliopigwa katika dimba la Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara
Bao pekee na la ushindi la timu ya Ndanda fc ambayo hii leo imefufuka baada ya kupotea kwa takribani michezo minne mfululizo limefungo na kiungo hodari wa timu hiyo Jackob Masawe,
Kule jijini Tanga wenyeji Coastal Union wameutumia vema uwanja wao wa nyumbani wa Mkwawani baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande wa Ruvu Shooting toka Mlandizi mkoani Pwani
Matokeo mengine ni katika uwanja wa Azam complex wenyeji maafande wa JKT Ruvu toka mkoa Pwani wamekubali kichapo cha bao 2-1 toka kwa maafande wa Polisi Morogoro, na katika uwanja wa kambarage mjini Shinyanga wenyeji Stand United wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na maafande wa magereza Tanzania Prisons toka mkoani Mbeya.
Ligi hiyo inataraji kuendelea tena kesho kwa mtanange mmoja utakaopigwa katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga baina ya wenyeji maafande wa Mgambo Shooting dhidi wagonga nyindo wa jiji la Mbeya timu ya Mbeya City.