Jumla ya vituo 2 vimewekwa mkoani Mtwara kuwezesha raia hao kufanikisha upigaji kura huo ambapo vyama 3 vimeweka mgombea urais chama cha Renamo, Frelimo na MDM, kituo kingine kipo mahurunga mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Wakizungumza wakati wa upigaji kura huo baadhi ya raia hao wa Msumbiji waishio mkoani Mtwara wamesema wamefurahi kuona serikali ya msumbiji imeweka utaratibu wa kuwawezesha wao walio nchini Tanzania kupiga kura, na kwamba hali hiyo inatokana na uhusiano mzuri kati ya nchi hizo 2.
Msimamizi wa kituo cha kupigia kura namba 4, Kizito Mmandamo amesema upigaji kura umeendelea vizuri, raia hao walianza kuja kituoni kuanzia saa 9 usiku na kwamba upigaji huo ni wa kumchagua Rais toka vyama vya Renamo, Frelimo na MDM ambapo kwa uchaguzi wa wabunge wapiga kura hukipigia chama ili kumpata mbunge, huku mwenyekiti wa jumuiya wa raia wa Msumbiji waishio mkoani Mtwara Bibi Regina Kaunda ameishukuru serikali ya Msumbuji kwa kuwahusisha masuala ya kitaifa raia wake, walioko nje ya nchi.
Huu ni uchaguzi mkuu wa 2 wa Msumbiji uliowashirikisha raia ya nchi hiyo waishio mkoani Mtwara kupiga kura, wa kwanza ulifanyika mwaka 2009, ambapo kwa sasa ikikadiriwa mkoa huo wa Mtwara kuwa na raia wa Msumbiji zaidi ya 4,500 wanaoishi mkoani humo.
Kwa upande mwingi, taarifa kutoka katika ubalozi wa Msumbiji inasema kuwa Zaidi ya Raia 12,000 wa Msumbiji waishio Tanzania wamepiga kura hiyo katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na ubalozi wa Msumbiji jijini DSM.