Jumatano , 15th Oct , 2014

Chama cha Walimu mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania kimeitaka Serikali kuwasilisha michango yao ya SACCOS kwani kuchelewesha huko kwa fedha zao kunafanya walimu kukimbilia katika taasisi zingine za kifedha kutafuta mikopo.

Akizungumza mjini Moshi, Katibu mkuu wa Chama hicho mkoa wa Kilimanjaro Bw. Nathanel Mwandete, amesema fedha hizo karibu sh. Bilion 1 za miezi miwili ambazo wanakatwa katika mishahara yao na Halmashauri kama michango ya SACCOS ni halali yao hivyo serikali haina budi kuzifikisha kwa wakati ili kuondoa usumbufu kwa walimu hao.

Mwandele amesema kitendo cha walimu kwenda kukopa kwenye taasisi nyingine kimekuwa kikiwaletea adha kubwa kutokana na riba kubwa na masharti magumu yanayowekwa na taasisi hizo, tofauti na taratibu zinazowekwa na SACCOS za walimu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Kilimanjaro amesema kuwa endapo ombi lao hilo la kufikishiwa fedha kwa wakati halitatekelezwa basi watawashawishi wanachama wao kuingia barabarani ili kudai haki zao hizo za msingi.