Uwanja wa Jamhuri ambapo patatumika kukabidhi Katiba inayopendekezwa pakiwa tayari pameandaliwa
Wakati Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Mrisho Kikwete akitarajiwa kukabidhiwa Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum kesho mjini Dodoma, maandalizi kabambe kwa ajili ya hafla hiyo yamefanyika mjini humo huku idadi kubwa ya wageni wakiwasili ambapo hali ya ulinzi imeimarishwa mara dufu kuelekea katika tukio hilo la kihistoria.
EATV imeshuhudia watu kwa makundi kutoka nje ya mji wa Dodoma yakiwasili huku katika eneo la uwanja wa Jamuhuri ambako tukio hilo litafanyika kumepambwa kwa majukwa na nakshi za aina mbalimbali sambamba na kufanyika kwa usafi na ulinzi wa hali ya juu.
Zaidi ya wageni 3000 wakiwemo viongozi wa kitaifa na makundi mbalimbali ya kijamii kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar wanatarajiwa kushuhudia tukio hilo la kihistoria ambapo jeshi la polisi mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wameimarisha ulinzi mara dufu katika viunga vya mji wa Dodoma ili kuhakikisha hali ya ulinzi inaboreka wakati wote kabla wakati na baada ya tukio hilo adhimu.
Mbali na Rais Kikwete ambaye ataongoza shughuli hiyo pia atakuwepo Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar pamoja na makamu wa Rais wote wa muungano na Zanzibar, waziri mkuu, waziri kiongozi na mawaziri wakuu na viongozi wote wastaafu wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania mabalozi wa nchi mbalimbali na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa.
Wakati huohuo mkoa wa Dodoma umefanya dua maalum ya kuliombea taifa amani katika kuelekea shughuli hiyo ambapo viongozi wa dini ya madhehebu mbalimbali wameongoza dua hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere vilivyoko katikati ya mji wa Dodoma.