Jumapili , 2nd Feb , 2020

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Salum Hamduni, amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka Mtume Boniface Mwamposa, aliyetoweka baada ya watu takribani 20 kufariki, wakati wakikimbilia kukanyaga mafuta katika kongamano lake lililofanyika mkoani humo.

Mtume Boniface Mwamposa, kulia ni RPC Kilimanjaro Salum Hamduni

Akizungumza leo Februari 2,2020 na EATV&EA Radio Digital, Kamanda Hamduni amesema kuwa hadi sasa Jeshi hilo linawashikilia watu Saba kwa mahojiano zaidi kufuatia tukio hilo na kwamba jumla ya watu 20 walipoteza maisha huku wengine 16 wakijeruhiwa.

"Hatua tulizozichukua hadi sasa ni kuanza uchunguzi wa kujua ni nini hasa kilitokea na kupelekea vifo na majeruhi kwa hao waumini na tunawashikilia watu saba kwa mahojiano, Mchungaji Mwamposa tunamtafuta kwakuwa alitoweka mara baada ya hilo tukio kutokea" amesema Kamanda Hamduni.

Kwa mujibu wa Kamanda Hamduni jumla ya watu 20 walipoteza maisha siku ya jana ya Februari 1, 2020, katika viwanja vya Majengo Mjini Moshi, ambapo Watoto wa kike ni Wanne, Wanawake 15 na Mwanaume ni Mmoja, na majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Mawenzi.