
Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu
Kesi hiyo imesikilizwa leo kwa njia ya mtandao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini ambapo upande wa Jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema umesema kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya Lissu kusomewa maelezo ya awali lezo ya Awali (Ph).
Hata hivyo, upande wa Jamhuri kupitia Wakili Mrema ulipouliza mbona Mshtakiwa Lissu haonekani mtandaoni, Hakimu Mhini alimtaka Askari Magereza ajibu ambapo alisema kwamba Lissu amegoma kusomewa maelezo ya awali kwa njia ya mtandao (visual) ambapo Hakimu Mhini aliruhusu kesi kuendelea pasipo Lissu kuonekana.
Katika kesi hiyo Lissu anatetewa na Jopo la Mawakili 31 wakiongozwa na Wakili Mpale Mpoki ambaye aliungana na Alute Mugwai, Peter Kibatala na Jeremiah Ntobesya kuwasilisha mapingamizi, miongoni mwa hoja kuu za mapimgamizi yao ni kwamba wanapinga utaratibu wa kesi hiyo kusikilizwa kwa njia ya mtandao huku wakitaka Mtuhumiwa afikishwe mahakamani kwani ili asomewe Maelezo ya Awali (Ph) lazima upande wa Jamhuri, Utetezi na Mtuhumiwa wawepo Mahakamani sambamba na mtuhumiwa kusaini karatasi ya maelezo.
Kesi ya Lissu imeahirishwa hadi Aprili 28, 2025 kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mapingamizi hayo ya utetezi kwa njia ya mtandao ili kuona kama kesi hiyo isikilizwe kwa mtandao ama mshtakiwa afikishwe Mahakamani.