Jumatano , 18th Dec , 2019

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt Bashiru Ally, akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Iringa, amewahakikishia wanachama wa CCM kuwa chama hicho hakipo tayari kupoteza jimbo la Iringa Mjini, kama ilivyofanyika miaka michache iliyopita.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt Bashiru Ally.

 

Bashiru ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Kamati za Siasa za Wilaya ya Kilolo, Iringa Mjini na Iringa Vijini mara baada ya kupokelewa  akitokea mkoani Dodoma.

"Ujumbe ninaoutoa kwa Vyama vya Upinzani, nataka jimbo la Iringa Mjini na Manispaa yake lirudi CCM, na Mkoa wa Iringa umekuwa ni ngome ya CCM miaka yote, hapa Mjini yalifanyika makosa ambayo ndani ya uongozi huu hayatojirudia tena." amesema Dkt Bashiru.

Aidha Katibu Mkuu ameongeza kuwa, Jimbo hilo lilipotea kutokana na migawanyiko ndani ya CCM, na atahakikisha Manispaa yake inarudi CCM na Chama hakitarajii kufanya makosa tena.

Katika hatua nyingine, Dkt Bashiru ameendeleea kuwaasa wanaCCM kuwa, heshima wanayopatiwa viongozi, ni heshima kwa Chama, ambapo ndani ya CCM hakuna mtu maarufu wala kiongozi maarufu kuliko chama.