
El Clasico ya Machi 2, 2019
Ni El Clasico, mchezo wa vigogo wawili wa Hispania, FC Barcelona na Real Madrid ambao kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Septemba 2019 na mtandao wa The Mirror, El Clasico ni mchezo wa nne kwa ukubwa na uhasimu duniani, jambo ambalo linatosha kukushawishi kutoukosa mchezo huu.
Jambo lingine ambalo linaleta hamu na joto la pambano hili ni kutokana na mwenendo wa timu hizi katika ligi kuu nchini Hispania La Liga, ambapo Barcelona inaongoza ligi ikiwa na pointi 35 sawa na Real Madrid lakini kinachovutia zaidi ni tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, Barca ikiwa juu kwa tofauti ya mabao mawili pekee dhidi ya Real.
Wengi wanaipa nafasi kubwa Barcelona kutokana na kikosi walichonacho ambacho kimeongezewa nguvu na Antoine Griezmann na Frank de Jong pamoja na uwezo wa fundi wa mpira na mchezaji bora duniani kwa sasa Lionel Messi, lakini kuibeza Real Madid ni kuikosea heshima hasa katika mechi hii.
Real imeonesha kuimarika sana katika siku za karibuni katika ligi tofauti na ilivyoanza msimu, ambapo katika michezo mitano ya mwisho imefanikiwa kuibuka na ushindi katika mechi nne, ikitoa sare mechi moja na hivyo kuifanya kuwa fiti kiakili na imani kuwa wanao uwezo wa kumshinda mpinzania wake hii leo.
Tangu Oktoba 2014, timu hizo zimekutana mara 21, Real Madrid ikishinda mara 9 huku Barcelona pia ikishinda mara 9 na michezo mitatu ikimalizika kwa sare.
Taarifa zinaeleza kuwa timu zote mbili zitatokea katika hoteli moja kuelekea uwanjani kutokana na sababu za kiusalama, ambapo baadhi ya mashabiki wanaosadikika kuwa ni wa jimbo la Catalonia wamepanga kufanya vurugu wakishinikiza uhuru wao. Ikumbukwe kuwa mchezo huo uliahirishwa mwezi Oktoba kutokana na sababu hizo za kiusalama.
Mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo, Barcelona ilishinda kwa bao 1-0 katika dimba la Santiago Bernabeu, bao pekee lililofungwa na Ivan Rakitic. Je, shuguli itakuwaje hii leo Camp Nou?