Alhamisi , 7th Mar , 2019

Takriban watu 50 waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Abood wamenusika kifo baada ya gari kuacha njia na kukigonga kituo cha mabasi yaendayo haraka kilichopo maeneo ya Kimara Kona Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es salaam.

Basi likiwa limeparamia kituo cha mwendokasi.

Mkuu wa Operesheni wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Trafiki), Abdi Isango amesema ajali hiyo imetokea leo Alhamis Machi 7,2019 saa 12: 30 asubuhi na chanzo chake ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo la Abood.

"Basi la Abood aina ya Marcopollo lilikuwa katika mwendokasi likimbizana na basi lingine. Lilipofika maeneo hayo lilitaka ku'overtake' basi la mbele yake lakini kutokana na kutokuwa makini wa kuacha nafasi alijikuta akiingia upande wa barabara ya mwendokasi na kuharibu miundombinu yake.

"Baada ya kuona nafasi ndogo kati ya basi jingine na ili asiligonge aliamua kuparamia barabara hiyo. Ameharibu nguzo za barabara hiyo na kituo pia gari lake kuharibika," amesema Isango.

Isango amesema kuwa hakuna madhara kwa abiria wa gari hilo na waliokuwamo katika kituo hicho na gari hilo limepelekwa Kituo cha Polisi Mbezi huku dereva wake akishikiliwa kwa mahojiano.