Jumatatu , 12th Nov , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo saa 10 jioni anatarajiwa kutoa maamuzi ya hatma ya zao la korosho, kama serikali watalinunua zao hilo, au watafanikiwa kumaliza mgogoro baina ya serikali na wafanyabiashara wa zao hilo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli

Mapema wiki iliyopita Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilitoa siku nne kwa wafanyabiashara wa zao la korosho kujitokeza kutaja kiasi cha kiasi cha tani ambacho watanunua kwenye korosho siku ambazo zinaisha leo.

Kufuatia tamko la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jumamosi ya Novemba 10 mwaka huu akiwa makao makuu ya Jeshi Rais Magufuli alikwenda kukagua magari ya ambayo yangeweza kutumika kubebea korosho kama wafanyabiashara wangekataa kuzinunua korosho.

Akizungumza na wanajeshi pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa nchini ambapo aliambatana na Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali Venance Mabeyo amesema "tumejifunza wametupa akili mapema wamechelewa na korosho zetu tutaziuza, na msimamo huu pia utaendelea kwenye mazao mengine kwa wale watakaotaka kuchezea wakulima, lazima tujipange kikamilifu."

"Waliokuwa wameomba wafanyabiashara kununua korosho  walikuwa zaidi ya 37, lakini waliojitokeza walikuwa zaidi 15 kwa hiyo walikuwa na mgomo tu ndiyo maana nilimuagiza Waziri Mkuu, atangaze siku nne mwisho jumatatu saa 10 jioni na kama hakuna atakayejitokeza tutaanzisha operesheni korosho, na tutazinunua zote na tutazisambaza wenyewe."

Maelfu ya wakulima wa nchini weamebakiza tumaini moja kutoka kwa serikali kufuatia wafanyabiashara hao kugomea, bei ya zao hilo ambapo serikali ilipanga kilo ianzie shilingi elfu 3, huku wafanyabiashara wakitaka 2700 kwa kilo moja.