Jumatatu , 29th Oct , 2018

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha kuwakamata, kuwahoji na kuwaachia kwa dhamana mbunge wa Busega (CCM), Dkt. Raphael Chegeni na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kwa madai ya kuharibu mali za mwekezaji raia wa Ujerumani.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha akipanda gari ya polisi.

Akizungumza na www.eatv.tv, Kamanda wa Polisi jijini Mbeya, Ulrich Matei amesema wawili hao walikamatwa, kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana, ambapo wao walipata taarifa kutoka katika ubalozi wa Ujerumani kwamba kuna watu wamevamia nyumba ya mwekezaji huyo mwenye mashamba ya parachichi.

Tulipopata taarifa kutoka ubalozi wa Ujerumani zilitushtua kwa sababu Tanzania ni nchi ya amani, hakuna matukio kama hayo ya kutumia mabavu, Masha na Chegeni walikuwa wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa Mahakama ya kumuondoa mwekezaji huyo katika eneo lile lakini walikosea kutumia njia ile", amesema Kamanda Matei.

Kamanda Matei amesema kuwa walipofika eneo la tukio walikuta Masha pamoja na wenzake wamefanya uharibifu wa baadhi ya vitu ikiwemo kuvunja nyumba ya muwekezaji wa zao la Parachichi Peter Cruise kinyume cha taratibu.