Jumatatu , 29th Oct , 2018

Mshambuliaji wa klabu ya Simba , Emmanuel Okwi ameweka historia nyingine msimu huu katika mechi ya ligi kuu Tanzania bara (TPL) dhidi ya Ruvu Shooting usiku wa jana, Oktoba 28.

Emmanuel Okwi akikabidhiwa mpira baada ya kufunga hat-trick

Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 ambapo mabao matatu kati ya hayo yakifungwa na mshambuliaji huyo raia wa Uganda.

Baada ya mabao hayo matatu, Okwi amekuwa mchezaji wa pili katika listi ya wafungaji wa hat-trick katika ligi kuu msimu huu, mwingine ni Alex Kitenge aliyefunga hat-trick dhidi ya Yanga Septemba 16 katika uwanja wa Taifa.

Rekodi nyingine aliyoiweka Okwi katika michezo yake minne ya mwisho ni ya kuongoza listi ya wafungaji bora wa ligi kuu mpaka sasa sawa na Eliud Ambokile wa Mbeya City. Okwi ana jumla ya mabao 7 aliyoyafunga katika mechi hizo nne mfululizo. Katika mchezo wa nyumbani wa Oktoba 6, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon, mchezo ambao Okwi alifunga bao lake la kwanza.

Mchezo uliofuata wa Oktoba 21, Okwi alifunga bao la pili katika ushindi wa Simba wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United kabla ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa Simba wa 5-0 dhidi ya Alliance, Oktoba 24. Hat-trick ya mchezo wa jana dhidi ya Ruvu Shooting imekamilisha idadi ya mabao hayo 8.

Okwi amekuwa na kiwango bora cha ufungaji katika uwanja wa taifa tangu msimu uliopita, ana kumbukumbu nzuri dhidi ya dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa kwanza wa ligi msimu uliopita, ambapo aliifunga mabao manne huku Simba ikiondoka na ushindi mnono wa mabao 7-0.