Jumamosi , 27th Oct , 2018

Madiwani wa Halmashauri ya Geita Mkoani Geita wamelazimika kugomea kikao cha baraza hilo kufuatia kutoelewana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Geita Elisha Lupuga, juu ya eneo itakalojengwa hospitali ya wilaya ya Geita.

Madiwani Halmashauri ya Geita wakiwa kwenye mgomo

Wakizungumza mara baada ya kutoka kwenye kikao hicho kilichovunjika kutokana na kutofikia muafaka, madiwani hao, walisikika wakilalamikia kupokonywa kwa mamlaka yao ya kujadili mipango ya halmashauri ikiwemo kujadili hospitali ya wilaya ikajengwe eneo gani.

Moja ya madiwani walisema “ajenda hii hata mimi, makamu mwenyekiti wa halmashauri sijui kwa sababu tulijua baraza la madiwani tutakaa ili tujadili hospitali itakaa wapi lakini ajabu leo tumeletewa waraka wa mahali pa kujenga hospitali.”

Diwani mwingine alisikika akisema “tumeamua kutoka nje, kwa sababu imekuja ajenda ya siri kwenye kikao inayoondeshwa na watu wachache ikiwa na nia ya kutupokonya mamlaka yetu ya kujadili mambo ya halmashauri.”

www.eatv.tv ilijaribu kumtafuta Mkuu wa wilaya ya Geita Herman Kapufi ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo lakini simu yake haikupatikana.