Alhamisi , 27th Sep , 2018

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Maua Sama amefunguka na kudai hatokuja kusahau mambo aliyoweza kuyapitia pindi alipokuwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi huku akiwashukuru mashabiki zake kwa kuweza kumpa ushirikiano kwa kipindi chote kigumu alichopitia.

Maua Sama

Maua Sama ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa twitter asubuhi ya leo mara baada ya kuachiliwa na Jeshi la Polisi kwa dhamana, Septemba 25, 2018 kutokana na kesi iliyokuwa inamuandama dhidi yake.

"Challenges ni njia  ya kutukuza na kutuongezea ufahamu wa mengine tusioyajua, ni ngumu sana kusahau nilioyapitia siku 10 zilizoisha juzi. zilikua ni siku ngumu zaidi  katika maisha yangu. Ila pamoja na yote nawashukuru sana kwa 'support' yenu kila mmoja kwa nafasi yake asanteni", ameandika Maua Sama.

Maua Sama alikamatwa na Jeshi la Polisi mnamo Septemba 16, 2018, kwa kutuhumiwa kudhihaki na kukejeli noti za fedha za kitanzania baada ya kusambaa 'video clip', iliyokuwa inawaonyesha watu wakicheza wimbo wake wa 'iokote' jambo ambalo ni kosa la jinai na kinyume na sheria kwa mujibu wa benki kuu.

Benki kuu ya Tanzania (BoT) siku ya Jumanne Septemba 18, ilitoa onyo kwa wananchi kuheshimu fedha ya Tanzania kwa kuwa ni moja ya alama ya taifa na kuonya kwamba kudhihaki na kukejeli noti na sarafu ni kosa la jinai.

"Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 26, BoT ndiyo taasisi pekee yenye mamlaka ya kutoa noti na sarafu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Benki Kuu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuharibu noti na sarafu (kifungu cha 28 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006", ilisema taarifa iliyotolewa na BoT.