mfano wa wanafunzi wa darasa la saba wakiwa wanafanya mitihani.
Hayo yameelezwa na mwalimu wa hesabati kutoka shule ya sekondari Makongo iliyopo jijini Dar es Salaam, Ndambwe Shabani wakati alipokuwa anazungumza katika kipindi cha EATVMjadala kinachorushwa na EATV, na kusema kuwa sio jambo zuri kwa wanafunzi hao siku ya leo kutumia muda mwingi kujisomea kwa maana wanachosha akili zao na badala yake amewataka wapumzike mapema ili kusudi waweze kufanya vizuri mitihani yao.
Aidha, mwalimu Ndambwe amesema kuna mambo mengi madogo madogo ambayo mwanafunzi pindi akiyafuata na kuyazingatia, yanaweza kumsababishia kufanya vizuri mitihani yake bila ya kukumbana na mkasa wa aina yoyote.
"Mwanafunzi anapaswa avae mavazi mazuri yasiyoweza kumuingiza kwenye matatizo na kumpotezea umakini wa kufanya mitihani, uchaguzi sahihi wa kujibu maswali, kuacha kula hovyo maana anaweza kujikuta anasinzia kwenye chumba cha mtihani, kuanza kufanya maswali marahisi na kumalizia yale magumu kusudi uendane na muda, kupitia kwa makini majibu yote uliyojaza kabla ya kukabidhi mtihani wako", amesema mwalimu Ndambwe.
Mbali na hilo, mwalimu Ndambwe ameendelea kufafanua baadhi ya mambo kuwa "msuli 'paper' kama wanavyoita wanafunzi wengi nchini, hauwezi kulipa katika kipindi hiki kwasababu mitihani inahitaji maandalizi makubwa. Kitu ulichoweza kusoma leo kichwa hakiwezi kuweka kumbukumbu ya kukuwezesha kufanya vizuri katika siku inayofuata".
Takribani watahiniwa 960,202 upande wa Tanzania Bara, wanatarajiwa kuanza mitihani yao ya taifa ya kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2018 hapo kesho, Jumatano huku idadi kubwa ikiwa ni wasichana.
Mitihani hiyo itafanyika kwa muda wa siku mbili ambapo kuanzia Septemba 5 na 6, 2018.