Jumamosi , 1st Sep , 2018

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ameitaka Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Septemba 16, 2018 ili kuepuka machafuko kwa kutotenda haki dhidi ya upande mmoja wa chama.

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye.

Sumaye ambaye ni mwenyekiti wa Chadema kanda ya Pwani na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi jimbo la Ukonga ametoa kauli hiyo leo Septemba Mosi, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa wao sio sehemu ya wafanya fujo lakini wanatoa tahadhari.

Tume haipaswi kupendelea upande wowote wa chama cha siasa, badala yake ihakikishe uchaguzi unafanyika bila kuonewa mtu, tumeshuhudia chaguzi nyingi zinaingia dosari ikiwemo mawakala kucheleweshewa barua zao huku wengine wakilalamikia kutangazwa mgombea ambaye hajashinda”, amesema Sumaye.

Sumaye ameongeza kuwa tume isiwe sehemu ya kuingiza watu kwenye matatizo, "Tunataka tume iwe huru isiogope kufanya kazi yao kwa ufasaha kwa sababu ya vitisho, sisi tunawahakikishia wananchi kuwa watadumisha amani na tutapokea matokeo kwa moyo mkunjufu ili mradi yawe ya haki”.

Uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo ya Korogwe Vijijini mkoani Tanga, Monduli jijini Arusha na Ukonga jijini Dar es salaam unatarajiwa kufanyika Septemba 16 baada ya mbunge mmoja kufariki na wengine wawili kujiuzulu.