Jumanne , 10th Jul , 2018

Baraza la soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limeahidi kushirikiana na (TFF), katika kufanikisha michuano ya kanda ya kuwania kufuzu fainali za AFCON kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, itakayoanza Agosti 11 hadi 26 mwaka huu jijini Dar es salaam.

Katibu mkuu wa CECAFA Nicolaus Msonye

Akizungumzia maandalizi kuelekea katika michuano hiyo itakayotumia uwanja wa Taifa na Chamazi,  Katibu mkuu wa CECAFA Nicholaus Musonye amesema, anaamini Tanzania itajitangaza vizuri kimataifa kupitia uandaaji wa mashindano makubwa ya soka ndani ya mwaka huu kama ilivyoanza na Kombe la Kagame.

''Kwa Tanzania kuandaa mashindano haya naamini ni fursa ya kuendelea kuandaa mashindano mengine makubwa yakiwemo CHAN na AFCON ya wakubwa na naiomba Serikali iendelee kusaidia kuhakikisha mashindano haya pia yanafanikiwa zaidi'', - amesema Msonye.

Michuano hiyo itashirikisha mataifa 10 na yamepangwa katika makundi mawili, ambapo mshindi wa jumla ataungana na Tanzania kushiriki michuano ya AFCON ya vijana kwa mwaka 2019 inayofanyika nchini kwa mara ya kwanza. Katika michuano hiyo Tanzania itawakilishwa na timu ya vijana (U17) Serengeti Boys, ambayo pia ilishiriki fainali hizo mwaka 2017 nchini Gabon.

Kundi A zimepangwa timu za Rwanda, Burundi, Somalia, Sudan na mwenyeji Tanzania huku kundi B likiwa na timu za Uganda, Kenya, Ethiopia, Sudani Kusini na Djibouti. Tanzania itafungua michuano hiyo Agosti 11 ikicheza dhidi ya Burundi.