Jumatano , 13th Jun , 2018

Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC, wamefanikiwa kuzikalisha timu zote nchini kwenye majina ya wachezaji walioteuliwa kuwania Tuzo ya mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika wa 2017/18 kwa kuingiza wachezaji watatu ambao wote kutoka ndani ya timu yao.

Hayo yamebainishwa Afisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo Juni 13, 2018 katika taarifa yake na kusema Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu (VPL), imeteua wachezaji watatu pekee kati ya 15 wa awali waliokuwa wanagombea kuingia katika tatu bora hiyo na kuenda kwenye mchakato wa kumpata mmoja.

"Wachezaji watatu waliobaki katika kinyang'anyiro hicho ni Emmanuel Okwi, John Bocco na Erasto Nyoni wote wa Simba, ambapo kamati ya Tuzo hiyo ya mchezaji Bora imeandaa utaratibu wa kupiga kura kuwashirikisha Wahariri wa Habari za Michezo, manahodha wa timu za Ligi Kuu na makocha wa timu za Ligi Kuu", imesema taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo pia imesema kamati imekamilisha uteuzi wa wachezaji watakaowania tuzo katika vipengele mbalimbali kwenye sherehe hizo za Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL itakayofanyika ukumbi wa Mlimani, City Dares Salaam Juni 23 mwaka huu.

Tuzo 16 zinatarajiwa kutolewa siku hiyo, ambapo baadhi ni za kikanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambazo tayari washindi wake wamefahamika, ambazo ni bingwa, mshindi wa pili, mshindi wa tatu, mshindi wa nne na mfungaji bora.