Jumatano , 31st Jan , 2018

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Esther Bulaya amesema bado lipo hitaji muhimu la kuwepo fao la kujitoa kwani linaweza kumtoa mwanachama kwenye umaskini wa kipato.

Esther Bulaya.

Mhe. Ester Bulaya ameeleza hayo leo Bungeni wakati alipokuwa anatoa maoni ya kambi hiyo baada ya kuwasilishwa muswada wa sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma wa mwaka 2017 ambao umelenga kuunganisha mifuko minne ya umma na kuwa mmoja wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma.

"Bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na fao la kujitoa kama ilivyokuwa linatolewa na mifuko iliyokuwapo ni la msingi na lazima. Kwani mwanachama anakuwa tayari na akiba yake na hivyo huo unakuwa ni mtaji wa kumtoa kwenye umaskini wa kipato", alisema Bulaya.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amesema lengo la kuunganishwa kwa mifuko hiyo ya pensheni ambayo ni PSPF, LAPF, GEPF na PPF ni kukidhi kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kuhusu kuunganisha mifuko hiyo ili kupunguza gharama za uendeshaji.