Jumanne , 26th Sep , 2017

Baada ya kuachana na kocha wake raia wa Malawi Kinah Phiri hatimaye klabu ya Mbeya City leo imepata mrithi wa kiti hicho cha benchi la ufundi.

Mbeya City imefikia makubaliano na kocha Nsanzurwimo Ramadhani kuwa kocha Mkuu kwa mkataba wa msimu mmoja wa ligi ambao una kipengele cha kuongezwa endapo atafanya vizuri.

Msemaji wa Mbeya City Shah Mjanja amethibitisha hilo na tayari kocha huyo ambaye ni raia wa Burundi yupo nchini na mchana huu anatarajiwa kusafiri kuelekea Mwanza tayari kwa kujiunga na timu ambayo ipo mjini Shinyanga kwaajili ya mchezo wa ligi dhidi ya Mwadui.

“Ni kweli timu yetu imepata kocha mpya ambaye amesaini mkataba wa awali wa mwaka mmoja na ataongezewa endapo atafikia malengo ambayo yapo kwenye mkataba, tayari yupo nchini na anasafiri na ndege ya mchana kwenda kanda ya ziwa kujiunga na timu”, amesema Mjanja.

Kocha Ramadhani amewahi kuwa kocha kwa nyakati tofauti katika vilabu mbalimbali kwenye nchi za Burundi, Rwanda, Botswana, Malawi, Uganda, na Afrika ya Kusini.