Watuhumiwa hao wakiondolewa mahakamani
Watuhumiwa nane (8) kati ya 16 wanaokabiliwa na kesi ya kuhusika ulipuaji wa bomu katika baa ya Night Pack ya jijini Arusha na mtandao wa kigaidi wamepandishwa tena kizimbani katika mahakama kuu kanda ya Arusha na kusomewa kwa mara ya pili mashtaka yanayowakabili.
Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka yanayowakabili mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Mustapher Siyani, akisaidiwa na wakili wa serikali Hellen Rwijag, na hawakutakiwa kujibu lolote kuhusiana na kesi inayowakabili.
Hata hivyo washtakiwa hao walimwomba hakimu kulitaka jeshi la polisi kuwasilisha mahakamani hapo mali zao zilizochukuliwa wakati wanakamatwa zikiwemo simu za mkononi Nguo na Viatu.
Hata hivyo habari kutoka mahakamani hapo zimeeleza kuwa baadhi ya vitu wanavyohitaji watuhumiwa hao hawawezi kupewa kutokana na kuwa sehemu ya ushahidi wa kesi inayowakabili .
Wakati watuhumiwa hao wanafikishwa mahakamani hapo ndugu na jamaa zao walifika kwa wingi wakitaka kuwaona hali iliyosababisha askari kufanya kazi ya ziada ya kuwadhibiti na kuimarisha ulinzi.
watuhumiwa hao wanakabiliwa na kosa kujihusisha na usajili, usafirishaji wa vijana kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata mafunzo ya uhalifu na ugaidi na kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 25 mwaka huu itakapotajwa tena.
Kundi la pili la washitakiwa wengine wa kesi ya kulipua bomu wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kesho tarehe 12/06/14.