
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa Ikwiriri mkoani Pwani wakati alipokuwa akielekea mkoani Lindi na Mtwara katika ziara yake ya kikazi ya siku nne.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo katika ziara yake mkoani Pwani, wakati akizungumza na wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja, ikiwa ni ziara yake katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Amepokea kero za wananchi katika maeneo hayo na kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha
"Najua mmezoea kusikia maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa njaa, sasa mimi nasema usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata chakula wakati mvua inanyesha Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa, ni lazima tufanye kazi, sasa hivi mvua zinanyesha limeni mazao ya chakula" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa Nangulukulu mkoani Lindi.
Pia Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi huu na pia amepiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani humo na ameahidi kutoa Shilingi Milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Somanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Mbunge wa Kilwa Kusini Suleiman Bungara(Bwege ) kutoka CUF katika eneo la Somanga wakati alipokuwa akielekea Nangulukulu katika ziara yake ya mikoa ya Kusini.
Mbali na hayo Rais Magufuli amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kujenga kituo cha mabasi cha Nangurukuru na pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mhe. Hamidu Bobali kuhakikisha anapeleka Daktari katika kijiji cha Mchinga Moja ili kutatua kero ya wananchi kukosa huduma ya matibabu.
Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake kesho tarehe 03 Machi, 2017 hapa Mkoani Lindi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimian na mbunge wa Kilwa Kaskazini Vedasto Ngombale (CUF) mara baada ya kuhutubia wananchi wa Nangulukulu mkoani Lindi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpatia msaada wa Shilingi milioni moja kijana Abdulrahman Khalid ambaye ni mlemavu wa miguu katika eneo la Mchinga-1 mkoani Lindi, Katikati(Mwenye shati la maua) ni Mbunge wa Mchinga Hamidu Bobali kupitia chama cha (CUF) ambaye ameahidi kumpatia mlemavu huyo kiasi cha Shilingi Milioni moja pia.