
Mugabe ambaye hakuhitaji Hilary Clinton ashinde uchaguzi uliofanyika mwaka jana, kwa mara ya kwanza amezungumzia utawala wa Trump na kusema alishangazwa na ushindi wa kiongozi huyo kutoka chama cha Republican.
Rais huyo wa Zimbabwe amesema kuwa sera hiyo ya Trump ni bora sana kwa sababu inazungumzia zaidi kuhusu uzalendo.
"Marekani iwe ya Wamarekani - katika hilo, nakubaliana naye. Zimbabwe iwe ya Wazimbabwe,". Rais Mugabe aliyasema hayo kwenye dondoo ambazo zimechapishwa katika gazeti rasmi la serikali hiyo la Herald.
Mugabe amesema kuhusu uongozi wa Trump kiongozi huyo apewe muda kwanza ili uwezo wake kuongoza taifa hilo kubwa udhihirike.
Mugabe ambaye kesho anatimiza miaka 93 amechaguliwa na chama chake cha Zanu-PF kuwania nafasi ya kuendelea kuongoza Zimbabwe mwaka ujao akiwa anatimiza miaka 94.