Jumatatu , 6th Feb , 2017

Jumla ya kete 299 za dawa za kulevya zimekamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kufanyika msako kwenye nyumba za  watuhumiwa 112 wa dawa za kulevya wanaoshikiliwa na jeshi hilo kwa muda wa siku 3 ambapo 12 kati yao wako tayari kufikishwa Mahakamani.

Wema Sepetu

 

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu waliokamatwa wakijiusisha na dawa za kulevya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Simon Sirro amesema, watuhumiwa 12 akiwemo muigizaji filamu Wema Sepetu wamehojiwa naa kukiri kutumia dawa za kulevya na kukutwa na vielelezo na kwamba watuhumiwa wengine 100 watafikishwa Mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Kuhusu Wema Sepetu, Kamanda Sirro amesema kuwa uchunguzi uliofanyika umethibitisha kuwa mrembo huyo anatumia dawa za kulevya, mara baada ya kufanya upekuzi nyumbani kwake na kukuta misokoto ya bangi pamoja na karatasi ambazo hutumika kusokotea bangi.

Kamishna Simon Sirro

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda ametoa siku 10 kwa watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya kujisalimisha katika kituo cha Polisi Kati, sambamba na kuwataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuwasilisha orodha ya wakazi wao wanajihusisha na matumizi ya na biashara ya dawa za kulevya.

Akitoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam, Mhe. Makonda amesema, muda wa siku 10 alioutoa utawahusu wenyeviti wa serikali za mitaa wote katika mkoa wake, wazazi wenye watoto wanaojihusha na dawa ya kulevya na watumiaji wenyewe kujisalimisha kwani oparesheni ya kumaliza matumizi na uuzaji wa dawa za kulevya Jijini Dar es Salaam, inaendelea.