Mwadini Ally wa Azam na Hussein Sharrif 'Casillas Munyama' wa Mtibwa Sugar. Hawa ni baadhi ya makipa wanaofanya mazoezi yao Kinondoni.
Kufuatia kumalizika kwa ligi kuu Tanzania Bara, walinda milango wa timu kadhaa za ligi hiyo wamejikusanya na kufanya mazoezi kwa pamoja katika uwanja wa Garden uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam chini ya makocha Adam Meja ambaye ni kocha wa makipa wa Coastal Union ya Tanga na Mussa Mubaya Moloto ambaye ni kocha wa makipa wa Villa Squad ya Magomeni jijini DSM.
Mmoja wa makocha wa makipa hao bwana Adam Meja ambaye pia ni kocha wa makipa wa klabu ya Friends Rangers ya jijini Dar es salaam, amesema kuwafundisha makocha wa klabu kubwa hapa nchini kumempatia uzoefu mkubwa.
Akaongeza kwamba amepata ujuzi wake kupitia kozi kadhaa alizopitia lakini pia kutoka kwa makipa wa zamani ambao kwa sasa ni makocha kama vile Juma Pondamali.
Kituo hicho kipo chini ya bwana Mussa Mubaya maarufu kama Troti Moloto ambaye amesema malengo ya kituo hicho ni kuwasaidia makipa chipukizi kwa kuwapa mbinu zitakazowaendeleza na pia kuwakutanisha na makipa wakongwe ili kubadilishana uzoefu.
Makipa hao pia wameunda timu yao maalumu ambayo hucheza mechi kadhaa za kirafiki, nahodha wa timu hiyo Ally Shomary Jumanne maarufu kama Ndizi amesema hivi karibuni walicheza na Muhimbili Veteran na baadaye mwezi huu wataenda Iringa kucheza na timu ya mkuu wa mkoa huo
Naye kipa wa Mtibwa Sugar ambaye ni mmoja wa makipa wanaofanya mazoezi mahali hapo, Hussein Sharifu maarufu kama Casillas Mnyama amesema kitendo cha makipa hao kufanya mazoezi ya kucheza nafasi za ndani kunawafanya wawe na uwezo mkubwa wa kudhibiti mpira na kutopata wakati mgumu pale wanaporudishiwa mipira na mabeki wao wakati wa mechi.