Jumanne , 8th Nov , 2016

Wamarekani leo wanapiga kura kumchagua atakayerithi kiti cha Rais Barack Obama huku kukiwa na ushindani mkali kati ya wagombea wawili, Hillary Clinton wa chama cha Democratic na Donald Trump wa chama cha Republican.

Hillary Clinton (Kushoto) na Donald Trump

Uchaguzi wa leo unafanyika baada ya wagombea wote wawili kukamilisha kampeni zao katika majimbo muhimu.

Katika kampeni yake ya Pittsburgh, Clinton amewataka wapiga kura kukumbatia kile alichokiita matumaini na kuwaleta watu pamoja, kusikilizana na kuheshimiana.

Clinton ambaye amekamilisha kampeni yake usiku wa manane huko North Carolina amesema, siyo suala la jina lake na mpinzani wangu kwenye sanduku la kura, ni aina ya nchi wanayoitaka kwa ajili ya watoto na wajukuu zao.

Kwa upande wake Trump akiwahutubia wafuasi wake huko Raleigh, North Carolina, ametaka kuungwa mkono katika vita yake ya kupambana na mfumo wa ufisadi.