Alhamisi , 25th Aug , 2016

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mh. William Ole Nasha ameagiza mrajisi wa vyama vya ushirika nchini kuwasimamisha kazi viongozi wa vyama 98 vya ushirika mkoani Mtwara ambao wamesababisha wizi na ubadhirifu wa shilingi bilioni 4 za wanachama

William Ole Nasha

Waziri Ole Nasha ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na EATV ilipotaka kujua utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kutaka wizara hiyo ichukue hatua kwa watendaji wabovu wa vyama hivyo na kusababisha hasara kubwa ya fedha kwa taifa.

Amesema sambamba na hilo serikali imeweka sheria mpya kwa vyama vya ushirika ya kudhibiti ubadhirifu wa fedha na kudhibiti wizi kwa kuweka mifumo maalum ya kuangalia mapato ya vyama vyote vya ushirika na kubuni njia bora ya kuendesha vyama hivyo ili visiendelee kuliingiza taifa hasara ya fedha ambazo kama zikikusanywa vizuri zitapelekwa kuboresha maisha ya watanzania.

Amesema sheria hiyo imeanza kutekelezwa na kuahidi kutowavumilia wale wote wanaoiba fedha za umma.