Jumatatu , 9th Feb , 2015

Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini linakutana leo kwa ajili ya kujadili migogoro mbalimbali iliyojitokeza katika michuano ya ligi kuu na ligi daraja la kwanza.

Akizungumza na East Africa Radio, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura amesema moja ya shauri litakalopitiwa leo ni lile la mchezaji wa Ruvu Shooting George Assey kumfanyia vitendo vya udhalilishaji mchezaji wa Yanga Amis Tambwe.

Wambura amesema, suala la mchezaji huyo lilishindwa kusikilizwa hapo awali kutokana na mchezaji huyo kuwa na udhuru kwani wakati anapewa taarifa na malalamiko yaliyowasilishwa mchezaji huyo alikuwa njiani kuelekea Jijini Mbeya kwa ajili ya mechi.

Wambura amesema, kamati ya nidhamu ni moja ya vyombo vya haki vya TFF hivyo haikuweza kumhukumu wala kumtia mchezaji huyo hatiani mpaka pale vitakapomsikiliza kwa kutoa utetezi wake na kuulizwa maswali lakini kama mtuhumiwa huyo anaona hataweza kabisa kufika anatuma utetezi wake kwa maandishi.