Alhamisi , 4th Aug , 2016

Polisi nchini Zimbabawe wametumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuyavunja maandamano ya kuipinga serikali katika mji mkuu, Harare.

Baadhi ya Wanafunzi waliojitokeza katika maandamano yalivunjwa na Polisi Jijini Harare

Polisi wamewapiga waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti kuhusu maandamano hayo jana na kuvunja kamera zao pamoja na kulishambulia gari lililokuwa limewabeba waandishi habari na kuvunja vioo vya gari hilo na kuzichukua komputa zao ndogo.

Awali polisi hao waliyavamia maandamano ya wanaharakati wanaopinga mgogoro unaoikumba sarafu ya nchi hiyo.

Kundi jingine la waandamanaji wanaojiita wahitimu wa vyuo vikuu wasiokuwa na ajira nalo lilijitokeza kuandamana kuelekea bunge la nchi hiyo wakiwa wamevalia mavazi ya kupokea shahada.

Vikosi vya usalama vimeimarishwa katika maeneo ya mji mkuu Harare ingawa hali imetulia.

Hali ngumu ya maisha inayosababishwa na kudorora kwa uchumi nchini Zimbabawe imesababisha ghadhabu na maandamano ya mitaani ya kila siku.