Alhamisi , 30th Jun , 2016

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys Bakari Shime ametamba kuing'oa Shelisheli kwa kishindo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa mwishoni mwa juma hili.

Nyota wa Serengeti Boys wakishangilia moja ya bao katika ushindi walioupata dhidi ya timu ya Taifa ya Misri.

Shime maarufu kama mchawi mweusi kutoka Tanga amesema amewaandaa vijana wake kisaikolojia na kuwapa maarifa ya namna ya kuondoka na ushindi wanapocheza wakiwa ugenini hivyo bila shaka anaamini watafuata maelekezo yake.

Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imeondoka saa 9 alfajiri ya leo kwenda visiwa vya Shelisheli kwa ajili ya kuwavaa wenyeji katika mchezo huo kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.

Serengeti Boys imeondoka na matumaini makubwa ya kuiondoa Shelisheli katika mbio hizo baada ya kuvuna ushindi mnono wa mabao matatu kwa sifuri katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shirikisho la soka nchini TFF limewataka watanzania kuiunga mkono timu hiyo ambayo ili ifuzu,inahitaji kusimama imara katika matokeo hayo ama kwa kupata sare ya aina yoyote, kushinda au ikitokea kupoteza, basi isifungwe zaidi ya mabao 2-0.