Ijumaa , 3rd Jun , 2016

Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, leo imemkabidhi Bendera ya Taifa, mwanadada Melisa John ambaye ndiye mwakilishi wa Tanzania kwenye Shindano la Airtel Trace Music Stars litakalofanyika jijini Lagos nchini Nigeria na kuhusisha nchi tisa.

Melisa John anayeiwakilisha Tanzania kwenye Shindano la Airtel Trace Music Stars (wa kwanza kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bi. Leah Kihimbi na Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando.

Bi. Melisa anaiwakilisha Tanzania baada ya kuibuka mshindi wa shindano hilo linaloendeshwa na Kampuni ya Simu za mkononi ya Airtel Tanzania, ambapo washiriki hutumia simu zao za mkononi kuimba nyimbo ambazo hupitiwa na majaji kabla ya kupatikana kwa mshindi kama anavyoeleza Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando.

Akizungumza kabla ya kumkabidhi bendera hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bi. Leah Kihimbi amemtaka Melisa kutambua kuwa ndiye mwakilishi wa Tanzania katika mashindano hayo na kwamba kufanikiwa kwake ndio mafanikio na sifa ya Tanzania.

“Sanaa ni Kazi, ajira na ni bidhaa yenye thamani kubwa..Muziki kama tanzu mojawapo ya sanaa ina nafasi kubwa katika kubadili maisha ya mtu na nchi kiuchumi endapo itatumika vizuri. Ile dhana kuwa kazi ya muziki ni kuburudisha imepitwa na wakati hivyo wanamuziki sasa ingieni kazini,” amesema Bi. Kihimbi.

Huku akionyesha umahiri wa sauti na uimbaji; Melisa ameishukuru kampuni ya Airtel na kwamba ushindi wake ni ishara ya uwepo wa vijana wengi wenye vipaji kama chake lakini wamekosa fursa ya kuendelezwa.

Melisa ambaye anaondoka keho kwenda nchini Nigeria, amewaomba Watanzania wazidi kumuombea kwa Mungu ili afanikiwe kwani kamwe hatowaangusha.

“Nawaomba mashabiki zangu na Watanzania kwa ujumla kunipigia kura kwa kutuma ujumbe mfupi wenye neno MEL kwenda namba 15594, kura yako ni muhimu na itachangia kunipa ushindi,” amesisitiza Melisa.