Ijumaa , 3rd Jun , 2016

Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezitaka Halmashauri zote nchini kuacha urasimu kwenye mchakato wa utoaji hati miliki sambamba na kuwapa wananchi elimu ya kutosha juu ya sifa na nyaraka muhimu zinazohitajika katika upatikanaji wa hati.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam, na Kamishna msaidizi wa Ardhi Bwana Idrisa Kayera alipokuwa akiongea na East Africa Radio na kuainisha kuwa wanapokea hati nyingi zisizo na uambatanisho wa nyaraka muhimu kutoka katika Halmashauri jambo linalopelekea ucheleweshwaji wa hatu hizo

Amesema Halmashauri zinatakiwa kutambua kuwa, Serikali inalenga kuongeza milki ya Ardhi kwa watanzania kote nchini hivyo kuchelewesha utaratibu wa kutoa hati ni kwenda kinyume na utaratibu ulioainishwa na wizara na kusisitiza kuwa ni vyema Halmashauri zikawasaidia wananchi katika uchakato wa kupata hati hizo.

Serikali inalenga kuhakikisha kuwa hati inawanufaisha wananchi katika shuguli mbalimbali ikiwemo kuwekeza katika miradi, dhamana katika taasisi za kifedha pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi

Kwa upande wa jiji la Dar es salaam, Kayera amesema serikali itatoa leseni za makazi kwa wakazi wa Buuruni, Mburahati na Tandale kutokana na maeneo hayo kujengwa bila mpangilio na kwa upande wa maeneo ya Makongo na Kimara upimaji utafanyika na baadae hati miliki zitatolewa

“Buguruni, Mburahati na Tandale watu wamebanana sana, hivyo tutatoa leseni ya makazi maana hakuna namna ya kuyapima yale maeneo kwakuwa wamejengwa bila utaratibu” Amesema Kayera.