Alhamisi , 12th Mei , 2016

Serikali imesema kuwa tatizo la maji limeendelea kuwepo nchini kutokana na miradi mingi ya maji kutokamilika kwa wakati kutokana na serikali kudaiwa na wakandarasi wa miradi hiyo ambao wengi wao walisitisha ujenzi wa miradi.

Naibu waziri wa TAMISEMI, Mhe Suleiman Jaffo.

Akizungumza leo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la kutokamilika kwa miradi ya Maji wilaya ya Korogwe, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe Suleiman Jaffo amesema kuwa kusimama kwa miradi hiyo kulitokana na serikali kudaiwa jumla ya shilingi bilioni 28.

Aidha, Mhe. Jaffo amesema tayari serikali imeshawalipa wakandarasi hao na kuanzia wakati wowote watarejea katika maeneo ya miradi hiyo ili kuimalizia ikiwa ni pamoja kuanzisha mingine mipya.

Mhe. Jaffo amesema kutokana serikali kuimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato serikali imekusanya fedha za kutosha ambazo zitaweza kuendelea miradi mbalimbali ikiwemo ya maji ili kumaliza tatizo la maji kwa wananchi.

Naibu Waziri Jaffo ametoa agizo kwa wakurugenzi na wahandisi wote wa wilaya kuepeleka risiti za wakandarasi wizara ya maji ili wafanyiwe malipo na kuendelea na kumalizia miradi ambayo ilisimama kutokana na uksoefu wa fedha.