Jumatatu , 4th Apr , 2016

Aliyekuwa Mbunge wa Vunjo Augustino Mrema amesema wamekubaliana na Mbunge wa sasa James Mbatia kwamba kesi ambayo alikuwa ameifungua Mrema iishe kwa maslahi mapana ya wananchi wa jimbo la Vunjo.

'Mrema ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na EATV kuhusiana na taarifa kwamba ameshindwa kesi ya uchaguzi wa jimbo la Vunjo aliyoifungua Mahakama Kuu Moshi''-Amesema Mrema

''Taarifa kwamba nimeshindwa kesi sii za kweli ambacho tumekifanya ni maelewano ya mimi na Mbatia kwamba kesi hii tunapoteza muda bure ambao kila mtu angefanya shughuli nyingine''-Amesisitiza Mrema

Mrema na Mbatia wamefikia uamuzi huo baada ya kesi hiyo kuanza hivi karibuni ambapo Mrema alikuwa anapinga ushindi wa James Mbatia kwamba Mbatia alitumia njia zisizo halali katika kuupata Ubunge wa Jimbo la Vunjo.

''Tumeenda mahakamani na kila kitu kimekuwa ''settled'' baada ya kuiandikia mahakama ''statement'' ya kuwa tumeridhia kwa pamoja kuisitisha kesi ambayo ilikuwa mbele yangu kwa ajili ya kufanya kazi nyingine kwa maslahi ya wananchi na Jaji ameridhia''- Amesema Mrema.

Aidha katika matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka 2015 Mbatia alishinda Ubunge katika jimbo hilo kwa jumla ya kura 60,187 aliyemfuata ni Innocent Shirima aliyepata kura 16,617 na Mrema alipata kura 6,416.