Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika jijini Dar es Salam kati ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa niaba ya serikali na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.
Akifafanua kuhusu mikataba hiyo, Waziri Nchemba amesema kuwa mkataba wa dola za Marekani milioni 4, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 9.5 ni msaada na mkataba wa dola za Marekani milioni 100, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 238 ni mkopo wenye masharti nafuu.
Amesema mradi wa PAMOJA uliosainiwa utasaidia kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wanawake pamoja na huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia Tanzania Bara na Zanzibar.
"Hili litatimizwa kupitia uimarishaji vikundi vya wanawake kwa kuwajengea ujuzi wa biashara na kuwaunganisha na fursa za masoko, kuongeza fursa za mikopo nafuu kwa vikundi vya wanawake, kuwaongezea upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia mifumo rasmi ya kifedha pamoja na kuimarisha huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia”, amefafanua Dkt. Nchemba,
Amesema mradi huo utawanufaisha moja kwa moja wanawake wapatao 319,850 na walengwa wengine 399,000, wakiwemo wanafamilia za wanufaika.
Amesistiza kuwa kukuza usawa wa kijinsia si suala la wanawake pekee bali ni msingi wa Taifa la kidemokrasia, lenye haki na linalostawi na kuongeza kuwa kuondoa tofauti za kijinsia kunaboresha uzalishaji na kuimarisha uhimilivu wa kiuchumi.