Ijumaa , 18th Mar , 2016

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara Yanga leo Jumamosi wanashuka dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kukipiga dhidi ya APR ya nchini Rwanda katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Wachezaji wa Yanga, Donald Ngoma na Simon Msuva nyuma wakijaribu kumpokonya mpira Abdul Rwatubyaye wa APR katika mchezo wa awali nchini Rwanda

Afisa habari wa shirikisho la Soka nchini TFF Baraka Kizuguto amesema, maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa kwa timu ya APR kuwasili hapo juzi pamoja na waamuzi ambao wanatokea nchini Shelisheli pamoja na kamishna ambaye ametokea nchini Afrika Kusini.

Kwa upande wake mshambuliaji wa Yanga Simon Msuva amesema wanaamini mchezo utakuwa mgumu kwani APR wanahitaji kufunga ili wasonge mbele pia wao kama Yanga wanahitaji kusonga mbele ila ushirikiano baina ya wachezaji utawasaidia kuweza kushinda.

Msuva amewaomba mashabiki kufika uwanjani kwa ajili ya kuipa timu sapoti kwani mashabiki ndiyo wenye uwezo wa kuwafanya wachezaji wakazidi kuongeza juhudi uwanjani.

Kikosi cha APR kimewasili hapo juzi kikiwa tayari kwa ajili ya mchezo huo ambapo katika mchezo wa awali uliopigwa Kigali nchini Rwanda Yanga waliweza kuibuka na ushindi wa bao 2-1 ambapo katika mchezo wa hapo kesho APR wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili waweze kusonga mbele huku Yanga nao wakitakiwa kushinda.

Kwa upande wa wapinzani wa Azam FC, timu ya Bidvest ya nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kuwasili leo jioni huku waamuzi pia wakiwasili leo kutokea Sudan Kusini.

Kizuguto amesema, maandalizi kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa majira ya saa tisa jioni yamekamilika kwa asilimia kubwa.