Jumatano , 3rd Feb , 2016

Zaidi ya kaya 500 katika manispaa ya Mtwara Mikindani zimeathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia usiku wa juzi kuamkia jana, na kupelekea wananchi wengi wa kaya hizo kupoteza mali zao na vyakula.

Mkuu Wilaya ya Mtwara Mikindani Fatma Salum Ally.

Akitoa tathmini ya mafuriko hayo, Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, amesema amejitahidi kuzungikia maeneo mbalimbali katika kata zote 18 za manispaa hiyo akiambatana na kamati ya maafa na kubaini kuwa hakuna maafa yoyote kwa binadamu wala nyumba ambayo imebomolewa na mvua hiyo zaidi ya upotevu wa mali na vyakula.

Aidha, amesema bado wilaya inafanya jitihada za kuandaa makazi kwa ajili ya wananchi watakaokosa hifadhi katika kata zao ambapo wametenga eneo katika Chuo cha Walimu Mtwara (TTC) ambalo lina uwezo wa kuhifadhi zaidi ya kaya 30 huku jitihada za kupata maeneo mengine zikiendelea kufanyika.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wanaoishi maeneo yaliyo karibu na mfereji mkubwa unaopeleka maji baharini ukianzia mtaa wa Kiyangu kata ya Shangani, walionekana kutoridhishwa na ubora wake na kudai kuwa umezidiwa na maji kiasi cha kuonekana kama bado hauna msaada kwa sababu maji bado yamefurika kwenye nyumba za watu.