Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima katika moja ya michezo ya timu hiyo.
Hatimaye baada ya kimya cha muda mrefu hii leo kiungo aliyetimuliwa na klabu ya Yanga Mnyarwanda Haruna Fadhil Hakizimana Niyonzima ameomba msamaha kwa klabu ya Yanga na kuahidi kutorudia kuikwaza klabu hiyo kwa namna yoyote.
Ikumbukwe mwezi uliopita, klabu ya Yanga ilitangaza kuvunja Mkataba na Nahodha huyo wa Rwanda kwa tuhuma za kukiuka vipengele vya Mkataba wake.
Lakini leo akiambatana na mkuu wa idara ya habari ya Yanga Jerry Muro katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani jijini Dar es Salaam, Niyonzima ameomba msamaha ili arejeshwe kundini.
Aidha, Niyonzima amesema kwamba kulitokea kutoelewana kimawasiliano na ofisi ya Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha kiasi cha kulifikisha suala hilo kwenye hatua hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro amesema kwamba suala la Niyonzima limefika katika uongozi mkuu wa klabu na lipo katika hatua nzuri.
Ingawa Muro hakuweza wazi, lakini inavyoonekana muda si mrefu Yanga itatangaza kuzika tofauti zake na mchezaji huyo na kumrejesha kundini rasmi.
Yanga SC ilitangaza kuvunja Mkataba na Niyonzima, baada ya kuchelewa kurejea klabuni kufuatia kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini Ethiopia Novemba.
Awali, Yanga SC ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye ilichukua maamuzi magumu.
Pamoja na Niyonzima kuwasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu ulijiaminisha kiungo huyo alidanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.
Ulibaini plasta gumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.
Na ikamnasa kwenye picha za video siku za karibuni ‘akijirusha’ sehemu mbalimbali za starehe ikiwemo kwenye onyesho la mwanamuziki Ali Kiba.
Haruna aliyezaliwa Februari 5, mwaka 1990 Gisenyi nchini Rwanda, alijiunga na Yanga SC mwaka 2011 akitokea APR ya kwao, ambako aliwasili mwaka 2007 akitokea Rayon aliyoichezea kwa misimu miwili baada ya kujiunga nayo akitokea Etincelles iliyomuibua mwaka 2005.