Jumatano , 13th Jan , 2016

Serikali imeagiza sampuli ya maji kutoka mgodi wa North Mara kuchunguzwa na baraza la taifa la mazingira ili kubaini madhara yake katika maisha ya watu, wanyama na  mazingira.

Serikali imetoa wiki mbili kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kuchukua sampuri za maji yanayotiririka kutoka mgodi wa North Mara na kutoa hadharani matokeo uchunguzi wake ikiwa njia moja wapo ya kumaliza kabisa kilio cha miaka zaidi ya kumi kuhusu madai ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo kuwa maji hayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa kwa binadamu vikiwemo vifo vya watu ,mifugo na kuathiri vyanzo vya maji katika maeneo hayo.

Naibu waziri wa nchi, ofisi ya makamu wa Rais, muungano na mazingira Mh Luhaga Mpina, ametoa agizo hilo baada ya kutembelea maeneo yote ya mgodi wa North Mara ikiwa ni pamoja na kukagua mabwawa makubwa yanayotumika kuhifadhi mabaki ya maji kutoka mgodi huo kisha kuzungumza na uongozi wa mgodi pamoja na viongozi mbalimbali ngazi ya wilaya, kata na vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo.

Katika taarifa yake, meneja mkuu wa mgodi huo Bw Gary Chapman, amesema pamoja na madai hayo ya wananchi, mgodi wake ni miongoni mwa migodi nchini inayozingatia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira hata kufikia hatua ya kupewa tuzo mbalimbali za kutoka mamlaka zinazojihusisha na uhifadhi wa mazingira.

Naye mkuu wa wilaya ya Tarime Groriuos Luoga, akizungumza mbele ya viongozi hao wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo, amemuomba kiongozi huyo kufikisha malalamiko ya fidia za nyumba za wananchi katika wizara ya nishati na madini ikiwa utekelezaji wa ahadi ya Rais John Pombe Magufuli katika kumaliza kabisa migogoro ya mara kwa mara inayotokea katika eneo hilo…