Jumapili , 20th Dec , 2015

TAASISI mbalimbali Nchini zimetakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kuendana na mabadiliko ya Nchi yaliyopo hivi sasa yanayofanywa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa tawala za Mikoa Serikali za mitaa na utawala bora -Tamisemi Suleiman Japho wakati akifunga mkutano Mkuu wa pili wa chama cha wafanyakazi wa taasisi za elimu ya juu Tanzania (THTU) uliofanyika Mkoani Tanga.

Naibu Waziri Japho amesema ni vyema kila mtu akawajibika katika nafasi yake ipasavyo na kuwafichua wale wanaotumia vibaya madaraka na mali za umma ili kulinusuru Taifa na kutotegemea misaada kutoka nje ya Nchi.

Amesema kila mtanzania alikuwa akitaka mabadiliko ya kweli na sasa yametimia ambayo yanaleta heshima kubwa kwa Nchi yetu na nje ya Nchi baada ya kupata Rais mwadilifu na mwenye kutetea haki za watanzania kwa kuzuia ufisadi na ufujaji wa pesa za umma uliokuwa ukifanyika hapo nyuma.

Naye Mwenyekiti wa THTU Yusuph Singo amesema wao katika chama chao wameamua kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kasi kubwa ya vitendo aliyoanza navyo kwani wanaliunga mkono swala zima la kupinga madawa ya kulevya kuingia Nchini sambamba na kupinga rushwa.

Ameongeza kuwa watajitahidi kuwa mabalozi wazuri wa Nchi hii na kueleza kuwa vijana wao wanaowafundisha katika vyuo vikuu mbalimbali wanazingati misingi na weledi ikiwa ni pamoja na kuendana na mabadiliko ili Nchi yetu iweze kuvuka hapa ilipo na kuijengea heshima kubwa ya Tanzania.