Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira
Akizungumza na East Africa Radio katika mahojiano maalum Mwenyekiti wa Chama hicho Mama Anna Mghwira amesema rais Dkt. John Magufuli ameanza na kasi pamoja na viwango ambavyo mawaziri wake wanahitajika kwenda navyo sambamba ili kuleta maendeleo na kutatua kero za wananchi kwa haraka.
Aidha Mama Anna amemshauri rais Magufuli kuteua mawiziri makini katika wizara nne nyeti zilizobaki ambazo zinabeba uchumi wa nchi katika kugundua matatizo na kuyatafutia ufumbuzi kwa haraka.
Katika hatua nyingine Mama Anna Mghwira ameonesha kusikitishwa kwake na siasa za uchaguzi wa mwaka 2015 na kusema zilikuwa ni za upepo wa kishabiki zaidi kuliko kuangalia agenda za maendeleo kama ilivyokuwa siasa za mwaka 2010.
Amesema baada ya mwaka huu kuisha watafanya tathmini za kichama na uchaguzi ulivyokwenda ili kujipanga vizuri kwa kuimarisha chama na kuanza mikakati ya kupata viongozi wengi zaidi uchaguzi ujao utakapofika.