Jumatano , 2nd Dec , 2015

Wafanyakazi 635 wa Mgodi wa Tanzanite One wanaofanyakazi katika machimbo ya Tanzanite Mererani Simanjiro wanatarajiwa kupunguzwa kazi kutokana na hali ya uzalishaji ya kampuni hiyo kuzorota.

Meneja wa uchimbaji wa kampuni Tanzanite One, Apolinary Modest

Uamuzi wa kupunguza wafanyakazi hao umefikiwa na uongozi wa mgodi huo kwa madai kwamba ni kudorora kwa hali ya kifedha kwa kampuni hiyo kunakosababishwa na hali ya uzalishaji wa madini.

Akitolea ufafanuzi mchakato wa zoezi hilo katika eneo la mgodi huo wa Tanzanite Mererani, Meneja wa uchimbaji wa kampuni hiyo Apolinary Modest amesema mpango wa kupunguza wafanyakazi unakwenda sambamba na kuhakikisha kunazingatiwa kwa vipengele vyote muhimu vitakavyolinda stahiki zao.

Kwa upande wake wakili wa kampuni hiyo Kisaka Mnzava ameongeza kwamba zoezi la kupunguza wafanyakazi sio geni na kwamba kampuni yao sio ya kwanza hivyo jambo la msingi ni kuhakikisha zoezi hilo haliendi kinyume na taratibu za kisheria kiwemo kuwashirikisha wafanyakazi wote.

Hata hivyo wafanyakazi wenyewe katika mgodi huo wakiwakilishwa na viongozi wa chama chao cha (TAMICO) wamekiri kupokea taarifa ya kuwepo kwa zoezi hilo na kwamba wako tayari kwa hatua mbalimbali lakini pia wameeleza hofu yao ya kupoteza stahiki zao.

Jumla ya wafanyakazi 635 kati ya 1284 wanatarajiwa kupunguzwa kazi baada ya hatua ya majadiliano ya msingi baina ya wafanyakazi na uongozi wa mgodi huo.