Wakazi wa majimbo ya Lushoto mkoani Tanga na Ulanga mkoani Morogoro, leo wanapiga kura kuchagua wabunge wao kufuatiwa kuahirishwa kwa zoezi hilo hapo awali, baada ya waliokuwa wagombea katika majimbo hayo kufariki dunia kabla ya uchaguzi mkuu.
Taarifa ya Tume ya Uchaguzi kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe, imesema kuwa uchaguzi katika majimbo hayo unakwenda sambamba na ule wa madiwani katika kata sita ambazo uchaguzi wake nao uliahirishwa kutokana na vifo vya wagombea.
Kawishe amezitaja kata zitakazopiga kura hii leo kuwa ni zile za Muleba, Uyole, Bukene, Msingi, Bomang'ombe, na Kasulu, huku akitoa wito kwa wananchi wa majimbo husika na kata husika kujitokeza kwenye vituo walivyojiandikisha ili kuweza kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.