Rais Kikwete akiwajulia hali watu majeruhi katika hospitali ya mkoa ya Morogoro
Rais wa Tanzania, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, amewatembelea majeruhi waliolazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, waliojeruhiwa baada ya kukanyagana kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mara baada ya mkutano wa kampeni kumnadi mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, ambapo watu wawili walipoteza maisha na 17 kujeruhiwa.
Raisi kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM taifa, ameambatana na mkewe mama Salma Kikwete hospitalini hapo, na kutoa pole kwa majeruhi hao, sambamba na pole kwa wafiwa.
Rais Kikwete amesema tukio hilo halina budi kutumika kama fundisho kwa mikutano inayoendelea, kwa milango mingi kutumika hasa panapokuwa na msongamano mkubwa wa watu, huku akishauri uwezekano wa kuiboresha zaidi hospitali hiyo ya rufaa na kuwa ya ghorofa badala ya kutafuta maeneo nje ya mji kwaajili ya kuanza ujenzi mpya.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, Dkt Ritta Lyamuya, amesema walipokea majeruhi 19 waliotokana na tukio hilo, na wawili akiwemo Grace George (42) na mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi mkundi, Ramadhani Abdalah (12) walifariki dunia.
Awali baadhi ya majeruhi walidai vibaka walisababisha tukio hilo baada ya kulifunga lango kuu la kuingilia jamhuri na kuzidisha msongamano, ambapo mgombea ubunge kwa tiketi ya ccm, Abdulaziz Abood alifika kuwajulia hali majeruhi hao usiku huo na kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu.
Nyumbani kwa marehemu Grace, katika kata ya Kilakala, watu umejitokeza kwaajili ya msiba huo, ambapo kaka wa marehemu,Elvis George na mwenyekiti wa mtaa wa Kilakala, Gabriel Gondo, wamedai kupokea kwa masikitiko kifo cha ghafla cha mpendwa wao…