Ijumaa , 10th Jul , 2015

Wagombea wa nafsi za udiwani katika kata zilizopo ndani ya halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani wametakiwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika kipindi cha kampeni na uchaguzi mkuu.

Mkuu Wilaya ya Mtwara Mikindani Fatma Salum Ally.

Rai hiyo imetolewa jana mkoani humo na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Salum Ally, wakati wa kikao cha kuvunja baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa manispaa hiyo.

Katika hatua nyingine Jumla ya shilingi milioni 143, 750, 000 zimetolewa kama mkopo kwa vikundi vya wanawake na vijana, na halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani kupitia mfuko wa maendeleo ya wanawake na vijana toka mwaka 2010 mpaka mwaka huu.

Hayo yamezungumzwa mjini Mtwara na aliyekuwa Meya wa manispaa hiyo, Selemani Mtalika, wakati wa hotuba yake katika kikao cha kuvunja baraza la madiwani, na kuwataka waliopata mikopo hiyo kuendeleza uadilifu ili kutoa fursa kwa wengine waweze kunufaika nayo.

Ameongeza kuwa kupitia mfuko huo, halmashauri imekuwa ikitoa mikopo kwa wajasiliamali wadogowadogo waliopo katika vikundi vya kiuchumi ili kuwawezesha kupata mitaji kwa ajili ya kuinua kipato chao.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa manispaa hiyo Limbakisye Shimwela, akizungumza kwa niaba ya watendaji wengine, amewaahidi waliokuwa madiwani na aliyekuwa Meya wa manispaa Seleman Mtalika, kuwa wataikuta salama ikiwa chini yake kwa wale watakaobahatika kurejea katika nafasi zao.