Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini Tanzania ( MOAT) kimesema iwapo serikali itavinyima vyombo vya habari uhuru wa kupata na kusambaza habari, haitokuwa inawatendea haki wananchi na wananchi watasononeka na kuhuzunika kwa serikali yao kwa kuwanyima haki yao ya kupata habari.
Akiongea katika mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa MOAT Dk. Reginald Mengi amesema watu wanapaswa kuelewa kuwa wamiliki wa vyombo habari hawatetei maslahi yao katika Muswada huu wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa 2015 bali wanawatetea wananchi.
Kwa upande wa baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari nchini wamesema kuwa katika hali ya sasa kuna mambo ambayo ni lazima yanapaswa kutafuta majibu yake, ikiwemo huu uharaka wa serikali kuipitisha sheria ya kubana vyombo vya habari na kuwafanya wananchi wakose haki yao ya msingi ya kupata habari.
Kwa upande wake mwanasheria wa MOAT Dkt. Damas Ndumbalo amesema kuwa ni vema serikali kuangalia kwanza na kuiweka maslahi mbele kwa jamii ya watanzania inayopokea huduma hizo za habari nchini na kuzingatia utawala bora na ufuataji wa sheria.