Jumanne , 28th Mei , 2024

Kamati ya mpito ya Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBRC) imesitisha pambano la kugombea mkanda wa WBO Afrika baina ya bondia Mtanzania Hassani Mwakinyo dhidi ya Mghana Patrick Allotey lililopangwa kufanyika Mei 31-2024 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo Mei 28, 2024, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya mpito  ya TPBRC, Alex Galinoma amesema  wamefanya uamuzi huo kutokana na uvunjaji wa mikataba pamoja na kukiukwa kwa vigezo na masharti kutoka kwa promota wa pambano hilo.

"Tumeamua  kuchukua uamuzi huo haraka baada ya kubaini muandaaji  wa pambano hilo kutotii majukumu ya kifedha ambayo yanajumuisha malipo yaliyosalia yanayohusiana na ada za mabondia waamuzi na wasimamizi wa ngumi ikiwemo ada za kuidhinisha leseni na majukumu mengine ya kifedha, amesema  Galinoma. 

Kwa upande mwingine, mjumbe wa mpito wa kamati ngumi za kulipwa nchini Irene  Mwasanga amesema wapo kwenye mikakati ya kuweka sheria kali dhidi ya wakuzaji wababaifu kwenye masumbwi ili kulinda hadhi ya mchezo huo.

Hili linakuwa pambano la pili ndani ya kipindi cha miezi 8 kupita kwa  bondia Hassan Mwakinyo kwa pambano lake kushindwa kufanyika baada ya pambano la Septemba 29-2023 dhidi ya Julius Indogo kushindwa kufanyika baada ya sintofahamu kutokea baina ya promota na bondia Mwakinyo.