Jumapili , 21st Jul , 2024

Kikosi cha wachezaji na viongozi wa JKT Tanzania FC kimeelekea Jijini Mbeya ambako kitaweka kambi ya siku 23 kwa ajili ya maandalizi ya ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2024.

Kikosi hicho kinachoongozwa na Mkuu wa msafara Luteni Said Lebba, ambaye ni Mkurugenzi wa mashindano,  kinajumuisha wachezaji 30 na viongozi 15.

Wachezaji watatu hawakuweza kuambatana na kikosi hicho kwa sababu mbalimbali ambao wanatazamiwa kuungana na wenzao huko Mbeya siku chache zijazo.

Wachezaji hao ni pamoja na Seif Bausi ambaye yupo kwenye timu ya Taifa ya beach soccer iliyoko kambini na kwa sasa iko Zanzibar kwa ajili ya mechi za  kirafiki, Khatib Kombo yupo Zanzibar katika mafunzo ya kijeshi na Salaam Hamis ambaye tayari taratibu za kuondoka kwake kutoka KVZ, Zanzibar zimekamilika, muda wowote ataondoka kuelekea Mbeya.

Kocha Mkuu, Hamad Alli amesema, lengo la kambi hiyo ni kufanya maandalizi ya kutosha katika kukijenga na kukiimarisha kikosi ili timu ifanye vizuri katika msimu huu wa ligi.

Hapo jana timu kuondoka kuelekea Mbeya, ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Enjoy Soccer Centre ya mchezaji wa zamani Mrisho Alfan Ngasa na kupata ushindi wa magoli 6-0.

Wafungaji wa magoli katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa NDC, Kunduchi, ni John Boko, Sixtus Sabilo, Charles Ilamfya, Ismail Kader (penalty) na Mohamed Bakari aliyefunga magoli mawili.

Afisa Mtendaji Mkuu, Jemedari Kazumari, amesema kwamba, msimu huu amelenga timu kuitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya 'Kichapo cha Kizalendo' kwa kuhakikisha inakuwa miongoni mwa timu bora ligi itakapomalizika.