Baadhi ya wachezaji wapya wa Yanga
Yanga iko nyumbani katika Uwanja wa Taifa leo kucheza na Ruvu Shooting, kwenye mchezo wa kwanza wa ligi.
Kuelekea mchezo huo, kocha Zahera amesema amewaambia wachezaji wake wapya kutodharau mechi yoyote, huku akisisitiza kuwa wachezaji wa Kimataifa ambao hawakucheza mechi za Klabu Bingwa Afrika kwa sababu ya vibali, wako fiti kucheza mechi za ligi.
"Nimewaambia wachezaji wote wapya kwamba hakuna hata siku moja Yanga inacheza mechi nyepesi, mechi zote ni ngumu", amesema kocha Zahera.
"Wachezaji wote ambao hawakupata leseni za kucheza mechi za CAF wote watakuwa na nafasi ya kucheza ligi. Wachezaji wote wako vizuri", ameongeza.
Yanga imerejea usiku wa kuamkia Jumatatu kutoka nchini Botswana ambako ilicheza mechi ya marudiano na Township Rollers na kufanikiwa kuvuka hatua ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa utofauti wa bao moja.